TANZANIA YASHIRIKI MKUTANO WA MAWAZIRI WA UMOJA WA AFRIKA

TANZANIA YASHIRIKI MKUTANO WA MAWAZIRI WA UMOJA WA AFRIKA

Naibu Waziri wa Fedha, Mshamu Ali Munde, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, ameongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Pamoja wa Mawaziri wa Umoja wa Afrika unaofanyika Abidjan, Ivory Coast , Julai 23 hadi 24, 2026.

Mkutano huo umewakutanisha Mawaziri wa Fedha, Biashara, Viwanda na Madini, pamoja na Magavana wa Benki Kuu na viongozi wa taasisi mbalimbali za Umoja wa Afrika, kwa lengo la kujadili mikakati ya kuharakisha maendeleo ya viwanda kupitia upatikanaji wa fedha, biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi.

Ajenda kuu za mkutano huo ni pamoja na kuongeza upatikanaji wa fedha kwa maendeleo ya viwanda, kuimarisha usimamizi wa deni la umma, kukuza masoko ya mitaji, kuongeza ushiriki wa sekta binafsi na kuimarisha biashara ya ndani ya Afrika kupitia Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA).

Kwa Tanzania, ushiriki katika mkutano huo unatoa fursa ya kuwasilisha mafanikio yaliyopatikana katika usimamizi wa uchumi, uhamasishaji wa rasilimali za ndani na jitihada za kuboresha mazingira ya uwekezaji na maendeleo ya viwanda, sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Mkutano huo unafanyika chini ya kaulimbiu ya “Kufadhili Maendeleo ya Viwanda Barani Afrika kwa Maendeleo Endelevu” , ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano wa nchi za Afrika katika kukuza viwanda, biashara na uwekezaji.