MWANANCHI AHOJI KUCHELEWA KWA MABORESHO YA SOKO LA SAMAKI MAKANYAGIO

MWANANCHI AHOJI KUCHELEWA KWA MABORESHO YA SOKO LA SAMAKI MAKANYAGIO

Swali kuhusu hatima ya maboresho ya Soko la Samaki Makanyagio limeibuliwa na mwananchi mmoja katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata hiyo, huku akitaka kujua sababu za kuchelewa kwa utekelezaji wa mradi huo licha ya taarifa za kuwepo kwa fedha za maendeleo.

Akijibu hoja hiyo, Diwani wa Kata ya Makanyagio, Erick Lazaro, amesema fedha kwa ajili ya mradi huo tayari zipo na kwamba suala la maboresho ya soko hilo limeendelea kupewa kipaumbele na viongozi wa kata pamoja na wadau wengine wa maendeleo.

Diwani huyo amesema wananchi wanapaswa kuwa na imani kwani mipango ya kuboresha soko hilo ipo na hatua mbalimbali zimekuwa zikifanyika ili kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa ufanisi.

Hata hivyo, ufafanuzi zaidi ulitolewa na Mtendaji wa Kata ambaye amesema fedha zilizopo kwa sasa haziwezi kukamilisha mahitaji yote ya mradi kwani  kipaumbele kikubwa katika maboresho hayo ni ujenzi wa chumba maalumu cha kuhifadhia samaki na  kutengeneza barafu.

Huku wananchi wakiendelea kusubiri utekelezaji wa ahadi hizo, viongozi wa Kata ya Makanyagio wameahidi kusimamia kwa karibu matumizi ya fedha zilizotengwa ili kuhakikisha maboresho yaliyopangwa yanatekelezwa kwa wakati. Ujenzi wa miundombinu muhimu ndani ya Soko la Samaki unatajwa kuwa hatua itakayosaidia kuongeza thamani ya mazao ya wavuvi, kuboresha mazingira ya biashara na kuchochea ukuaji wa uchumi wa wananchi wa eneo hilo.