IGP WAMBURA ATAJA NJIA MPYA YA UKUSANYAJI WA USHAHIDI

IGP WAMBURA ATAJA NJIA MPYA YA UKUSANYAJI WA USHAHIDI

Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Camillius Wambura, amewataka watendaji wa Kamisheni ya Uchunguzi wa Kisayansi kufanya kazi kwa kuzingatia nidhamu, uadilifu na kujifunza kila wakati ili kukabiliana na mabadiliko ya sayansi na mbinu mpya za wahalifu.

Akizungumza leo Jumatatu, Juni 1, 2026 katika Shule ya Polisi Tanzania, Moshi mkoani Kilimanjaro, Wambura amesema uchunguzi wa kisayansi unahitaji umakini, weledi na kufuata taratibu zote za kitaaluma kwa kuwa kosa dogo linaweza kuharibu ushahidi na kuathiri mwenendo wa kesi mahakamani.

“Polisi wakilinda ukweli, wananchi wanapata haki,” amesema Wambura akisisitiza umuhimu wa uadilifu katika uchunguzi wa kisayansi.
Aidha, amesisitiza kuwa ukweli ndiyo msingi mkuu wa taaluma hiyo, hivyo ushahidi haupaswi kupotoshwa, kufichwa wala kuathiriwa na masilahi binafsi au ushawishi wowote.

Amesema maofisa wa uchunguzi ni sauti ya ukweli kwa waathiriwa, watuhumiwa, mahakama na jamii, hivyo wanapaswa kulinda uaminifu wa Jeshi la Polisi. Pia amewahimiza kuendelea kujifunza kwa sababu teknolojia na mbinu za kihalifu hubadilika kila siku.