VIKUNDI 28 IRINGA MJINI VYALAMBA SH MILIONI 402

VIKUNDI 28 IRINGA MJINI VYALAMBA SH MILIONI 402

 Ndoto za mamia ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika Manispaa ya Iringa za kujikwamua kiuchumi zimeendelea kupata uhai baada ya Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kukabidhi mikopo ya Sh milioni 402.26 kwa vikundi 28 vilivyokidhi vigezo, huku Mbunge wa Iringa Mjini, Fadhili Ngajilo, akitekeleza ahadi ya Sh milioni moja kwa Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Kusikia mkoani Iringa.

Hafla hiyo, iliyoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta, imekuja wakati Serikali ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan ikiendelea kusisitiza uwezeshaji wa wananchi kupitia mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri, hatua inayotarajiwa kuongeza ajira, kukuza biashara ndogo na kuimarisha uchumi wa kaya.

Mbali na vikundi hivyo kukabidhiwa hundi za mikopo, Mbunge Ngajilo alikabidhi Sh milioni moja taslimu kwa Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Kusikia, akitimiza ahadi aliyoitoa mbele ya wananchi wakati wa mkutano wa hadhara ulioongozwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, uliofanyika hivi karibuni mjini Iringa.

Hatua hiyo ilipokelewa kwa furaha na wanachama wa chama hicho, wakisema msaada huo utawasaidia kushiriki mkutano wao wa kitaifa unaotarajiwa kufanyika mjini Tanga baadae mwaka huu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Ngajilo alisema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha fedha za mikopo zinakuwa mtaji wa kuondoa umaskini badala ya kubaki kwenye akaunti za halmashauri.

“Tunataka fedha hizi ziwafikie wananchi, ziongeze mitaji ya biashara na zijenge uchumi wa familia. Tunawaomba wanufaika wazitumie kama zilivyokusudiwa na wazirejeshe kwa wakati ili na wengine wanufaike,” alisema.

Alibainisha kuwa, licha ya Manispaa ya Iringa kutokuwa na mapato makubwa ikilinganishwa na baadhi ya halmashauri nchini, imeendelea kutekeleza kwa ufanisi agizo la Serikali la kutenga fedha kwa ajili ya mikopo ya makundi maalumu.


Ngajilo alisema hatua hiyo inaendana na uamuzi wa Bunge uliopitisha ongezeko la fedha za mikopo ya makundi maalumu kutoka asilimia 10 hadi asilimia 15 ya mapato ya ndani ya halmashauri, hatua inayotarajiwa kuongeza fursa za uwezeshaji kwa wananchi.