WADAU WAASWA KUSIMAMIA MIRADI KWA UADILIFU KATAVI

WADAU WAASWA KUSIMAMIA MIRADI KWA UADILIFU KATAVI

Serikali mkoani Katavi imewataka wadau wa usimamizi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo kufanya kazi kwa uadilifu, uwazi na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma ili kuhakikisha miradi yote inatekelezwa kwa wakati na kutoa manufaa yaliyokusudiwa kwa wananchi.

Agizo hilo limetolewa leo Juni 30,2026 katika warsha ya wadau wa usimamizi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo na Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Mhe. Majid Mwanga aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe. Mwanamvua Mrindoko.

Amesema warsha hiyo inapaswa kuwa chachu ya kuongeza ufanisi katika usimamizi wa miradi na kutimiza maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Rai yetu kama mkoa ni kuhakikisha kila mmoja anatumia fursa hii kama nyongeza na chachu ya kufanya kazi kwa uadilifu ili dhamira na maono ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yafikiwe kwa wakati,” amesema Mhe. Mwanga.

Amesema maeneo yenye vitendo vya rushwa, ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka husababisha utekelezaji wa miradi kusuasua, hivyo amewataka washiriki kutumia maarifa watakayopata katika warsha hiyo kuziba mianya yote ya rushwa, matumizi mabaya ya fedha za umma na kuhakikisha maendeleo yanapatikana kwa kasi.

Aidha, amewasisitiza  watumishi wa umma kuzingatia maadili ya utumishi na kuwa mabalozi wazuri wa kuijenga nchi kupitia usimamizi madhubuti wa miradi ya maendeleo.

Kwa upande wake, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Katavi, Bi. Sifa Mwanjala, amesema Serikali imeendelea kuwekeza rasilimali nyingi katika programu na miradi mbalimbali ya maendeleo, hivyo kuna wajibu wa kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa uadilifu, uwazi na kwa kuzingatia thamani halisi ya fedha.

“Rushwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo husababisha hasara kubwa kwa Serikali na jamii kwa ujumla kwa kuchochea ujenzi wa miradi isiyo na viwango, kuongeza gharama zisizo za lazima, kuchelewesha utekelezaji wa miradi na wakati mwingine kukwamisha huduma zilizokusudiwa kuwafikia wananchi,” amesema Bi. Mwanjala.

Ameongeza kuwa mapambano dhidi ya rushwa ni msingi muhimu wa kuhakikisha miradi ya maendeleo inaleta tija, kuongeza imani ya wananchi kwa Serikali na kufanikisha maendeleo endelevu nchini.