UWAJIBIKAJI WA KILA MMOJA WATILIWA MKAZO KATIKA USAFI WA MAZINGIRA

UWAJIBIKAJI WA KILA MMOJA WATILIWA MKAZO KATIKA USAFI WA MAZINGIRA

Viongozi wa serikali na wananchi katika Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi, wametakiwa kutambua kuwa usafi wa mazingira ni jukumu la kila mmoja, ili kuhakikisha maeneo ya makazi yanakuwa salama na kuepuka madhara yanayotokana na uchafuzi wa mazingira.

Wito huo umetolewa katika kikao cha wadau wa mazingira kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Mpanda, ambapo washiriki walijadili mikakati mbalimbali ya kuboresha usafi na mifumo ya ukusanyaji taka.

Akiwasilisha mada katika kikao hicho, Godfrey Mbunda amejikita katika kuzungumzia uhifadhi wa mazingira na udhibiti wa taka ngumu, ambapo amesema mafanikio ya jitihada hizo yanategemea uwajibikaji wa viongozi wote wa serikali katika kusimamia sheria, pamoja na ushirikiano wa karibu kutoka kwa wananchi.

Sambamba na hilo, sekta binafsi zimeendelea kuunga mkono jitihada hizo huku Kikundi cha Trans Cargo kimezindua rasmi kampeni maalum ya usafi inayolenga kuzifikia kata kumi za Manispaa ya Mpanda ili kuboresha huduma za ukusanyaji taka.

Hata hivyo, baadhi ya wadau wameeleza kuwepo kwa changamoto ya ubaguzi wa maeneo katika upatikanaji wa huduma za ukusanyaji taka, Wamedai kuwa magari ya kubeba taka yanatoa huduma zaidi katikati ya mji, huku kata zilizoko pembezoni zikiachwa nyuma.

Kufuatia changamoto hiyo, kikao kimehimiza kuimarishwa kwa usimamizi ili kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma kwa usawa bila ubaguzi wa maeneo wanayoishi.