UJERUMANI YAFUNGISHWA VIRAGO KOMBE LA DUNIA 2026

UJERUMANI YAFUNGISHWA VIRAGO KOMBE LA DUNIA 2026

Timu ya taifa ya Ujerumani, Die Mannschaft, imeondolewa kwenye Kombe la Dunia 2026 baada ya kufungwa na Paraguay katika hatua ya mtoano. Matokeo hayo yamezua maswali mapya kuhusu mustakabali wa soka la Ujerumani.

Timu ya taifa ya Paraguay imefuzu hatua ya 16 bora baada ya kuiondoa Ujerumani kwa ushindi wa mikwaju ya penalti 4-3, kufuatia sare ya 1-1 iliyodumu hadi mwisho wa dakika 120 katika mchezo wa hatua ya mtoano uliochezwa mjini Boston, Marekani.

Ujerumani, ambayo ilikuwa ikipewa nafasi kubwa ya kushinda mchezo huo, ilitawala umiliki wa mpira kwa muda mrefu lakini ilishindwa kupenya safu imara ya ulinzi ya Paraguay.


Paraguay ilitangulia kupata bao kunako dakika ya 42 kupitia Julio Enciso. Hata hivyo baada ya mapumziko, Ujerumani Die Mannschaft ilisawazisha kupitia Kai Havertz kunako dakika ya 54 baada ya kupokea krosi safi kutoka kwa Florian Wirtz.

Pamoja na mashambulizi mengi ya Ujerumani katika kipindi cha pili na muda wa nyongeza, walishindwa kupata bao la ushindi kutokana na uimara wa Paraguay na ubora wa kipa Orlando Gill.


Dakika za nyongeza zilikuwa na patashika baada ya Jonathan Tah kufunga bao ambalo lingeipa Ujerumani ushindi, lakini mwamuzi alilifuta kufuatia mapitio ya VAR yaliyobaini kulikuwepo na madhambi kabla ya Jonathan Zah kuutia mpira kambani.

Katika mikwaju ya penalti, Ujerumani ilikumbwa na presha kubwa huku Kai Havertz, Nick Woltemade na Jonathan Tah wakishindwa kufunga mikwaju yao. Kipa wa Paraguay, Orlando Gill, aliibuka shujaa kwa kuokoa penalti muhimu, kabla ya José Canale kufunga mkwaju wa ushindi na kuipeleka Paraguay hatua inayofuata ya mashindano hayo.