SERIKALI KUIMARISHA MFUMO WA MAONI KUBORESHA UBORA WA HUDUMA ZA AFYA NCHINI

SERIKALI KUIMARISHA MFUMO WA MAONI KUBORESHA UBORA WA HUDUMA ZA AFYA NCHINI


Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea kutafuta njia bora za kupokea na kufanyia kazi maoni ya wananchi kuhusu huduma wanazopata, ili kuimarisha ubora wa huduma za afya nchini.

Akizungumza mbele ya Kamati ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI jijini Dodoma, Oktoba 20, 2026, Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Bruno Sunguya amesema maoni ya wananchi ni nyenzo muhimu katika kubaini mapungufu ya huduma na kuwezesha hatua za maboresho kuchukuliwa kwa wakati.

Amesema Serikali inatambua umuhimu wa kuwepo kwa mifumo rahisi na inayofikika ya kupokea mrejesho, ikiwemo matumizi ya majukwaa ya kidijitali yatakayowawezesha wananchi kutoa maoni kuhusu huduma walizopata katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Prof. Sunguya ameeleza kuwa mfumo huo unaweza kuruhusu wananchi kutoa maoni kwa usiri au kwa kutumia taarifa zao pale inapohitajika, ili kuwapa uhuru wa kueleza uzoefu wao bila vikwazo visivyo vya lazima.

Prof. Sunguya amesema si kila changamoto inayojitokeza katika utoaji wa huduma hufikishwa kwenye mabaraza ya kitaaluma, hivyo ni muhimu kuwa na njia nyingine za kupokea taarifa zinazoweza kusaidia kutatua mapungufu ya kiutendaji katika ngazi husika.

Amesisitiza kuwa mrejesho unaopokelewa unapaswa kufanyiwa kazi na kufikishwa kwa wahusika kwa wakati, kwa kushirikiana na taasisi zinazohusika, ili hatua za maboresho zichukuliwe na kuongeza imani ya wananchi kwa huduma zinazotolewa.

Aidha, amesema juhudi hizo zitaendelea kuunganishwa na maboresho ya mifumo ya utoaji wa huduma za afya, ikiwemo utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma unaenda sambamba na ubora unaotarajiwa na wananchi.

Katika hatua nyingine, Prof. Sunguya amemshukuru Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dkt. Zeyana kwa ushauri wake wa kutumia njia za kidigitali ili kuwa na mfumo wa utoaji wa taarifa na maono kwa wananchi