MGONJWA WA KWANZA WA EBOLA APONA MJINI BENI

MGONJWA WA KWANZA WA EBOLA APONA MJINI BENI

                                                  

Mji wa Beni, ulioko mashariki mwa Kongo, umepiga hatua hatua muhimu katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ebola baada ya Charline Kavira Mukelu kuwa mgonjwa wa kwanza kuthibitishwa kupona ugonjwa huo.

Kupona kwa mgonjwa huyo kunatajwa kuwa ishara ya matumaini kwa wakaazi wa eneo hilo, ambao kwa miaka mingi wameathiriwa na milipuko ya mara kwa mara ya Ebola pamoja na changamoto za kiusalama zinazoathiri utoaji wa huduma za afya.

Serikali ya Kongo, kwa ushirikiano na wadau wa kimataifa, inatarajia kufungua kituo kipya cha matibabu ya Ebola katika mji wa Beni.


Kituo hicho kinatarajiwa kuongeza uwezo wa kupokea wagonjwa, kuboresha huduma za matibabu, na kuimarisha ufuatiliaji wa maambukizi katika mikoa iliyo hatarini.


Mji wa Beni umewahi kuwa kitovu cha mlipuko mkubwa wa Ebola kati ya mwaka 2018 hadi 2020, mlipuko uliosababisha maelfu ya maambukizi na kuacha athari kubwa za kiafya, kijamii na kiuchumi. Changamoto za kiusalama, uhamaji wa watu, na udhaifu wa miundombinu ya afya zilichangia kuongezeka kwa kasi ya maambukizi katika kipindi hicho.


Mlipuko wa sasa unatofautiana na ile ya miaka ya nyuma kwa sababu unasababishwa na kirusi cha Bundibugyo, ambacho ni nadra ikilinganishwa na kirusi cha Zaire kinachojitokeza mara nyingi zaidi.


Tofauti hii imeleta changamoto katika utambuzi wa ugonjwa huo, kwani kwa wiki kadhaa maambukizi yalikuwa hayagunduliki kwa usahihi kutokana na vipimo vilivyoelekezwa zaidi kwenye kirusi cha Zaire.