MAELFU YA WAHAMIAJI WAONDOKA AFRIKA KUSINI KABLA YA JUNI 30

MAELFU YA WAHAMIAJI WAONDOKA AFRIKA KUSINI KABLA YA JUNI 30

Maelfu ya wahamiaji wanaendelea kuondoka Afrika Kusini kufuatia kuongezeka kwa matukio ya chuki na mashambulizi dhidi ya raia wa kigeni, hali ambayo imezua taharuki kubwa katika maeneo mengi ya nchi hiyo.

Wimbi hilo la uhamaji limetokea sambamba na maandamano na mikutano kadhaa iliyoandaliwa katika miezi ya hivi karibuni na makundi yanayopinga uhamiaji, ambayo yamekuwa yakitoa matamko ya chuki dhidi ya wageni.

Makundi hayo yameweka tarehe 30 Juni kama muda wa mwisho kwa watu wanaoishi nchini humo bila vibali halali kuondoka, na yanaitaka serikali ichukue hatua kali dhidi ya kile yanachokiita ongezeko la uhamiaji haramu katika taifa hilo lenye uchumi mkubwa zaidi barani Afrika. Kauli hizo zimeibua hofu kubwa miongoni mwa wahamiaji, ambao wengi wao wanasema hawajisikii tena salama katika jamii.


Kwa mujibu wa Waziri wa Usalama wa Ndani, mamlaka za Afrika Kusini ziko katika hali ya tahadhari ya juu, hasa ikizingatiwa kuwa makundi hayo yanapanga kufanya maandamano makubwa zaidi kesho Jumanne. Serikali imesema inafuatilia kwa karibu mienendo ya makundi hayo ili kuzuia machafuko na kulinda usalama wa raia wote.


Katika maeneo mbalimbali ya mijini, maelfu ya wahamiaji wamekusanyika katika makazi ya muda, karibu na ofisi za balozi zao na maeneo mengine yenye ulinzi, wakisema wanaishi kwa hofu ya kushambuliwa. Wengi wao wanatoka mataifa kama Zimbabwe, Malawi, Msumbiji, Ethiopia, Somalia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Baadhi ya nchi za Afrika zimeanza kuwaondoa raia wao kwa ndege za dharura, huku zikitoa kauli kali dhidi ya serikali ya Afrika Kusini kwa kile wanachosema ni kuongezeka kwa chuki dhidi ya wageni na kushindwa kudhibiti mashambulizi hayo. Serikali ya Afrika Kusini imekanusha madai hayo, ikisema inafanya kila juhudi kuhakikisha usalama wa watu wote wanaoishi nchini humo bila kujali uraia wao.